Shindano la hadithi fupi mzunguko wa tatu: Kifungilo yaibuka kidedea

Kinyang’anyiro cha kumpata mshindi wa shindano la kuandika hadithi fupi kwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini – Andika na Soma, linaloendeshwa na taasisi ya usomaji na maendeleo – Soma chini ya udhamini wa ubalozi wa Denmark  kimefanyika mwishoni mwa wiki tarehe 14/10/2016.

Katika tukio hilo mwanafunzi Eliana Ludovick Swai wa shule ya sekondari ya wasichana Kifungilo iliyoko Lushoto mkoani Tanga aliibuka mshindi kwa kuwabwaga wenzake 107 waliowasilisha hadithi zao, na 20 walioingia kwenye kinyang’anyiro cha kumpata mshindi; hivyo kujinyakulia kitita cha shilingi laki tano (500,000/=) na vitabu vyenye thamani ya shilingi laki tano.

Mashindano ya mwaka huu yalidhaminiwa na ubalozi wa Denmark.

Akizungumzia ushindi wake katika hali ya furaha na kutokuamini  Eliana amemshukuru sana Mungu, na walimu wake kwa kumjengea uwezo na hatimaye kuibuka mshindi. pia ameahidi kuendelea kujituma zaidi ili kuhakikisha anafika mbali.

Nafasi ya pili imeenda kwa Maria Makasi kutoka Jangwani sekondari na Seif Ibrahim Chekanae wa Tambaza sekondari zote za jijini Dar es salaam. washindi hawa wamejinyakulia zawadi ya kitita cha shilingi laki tatu (300,000) na vitabu vyenye thamani ya shilingi laki tatu (300,000) kila mmoja.

Aidha nafasi ya tatu imeenda kwa Jackline Richard Kisanga wa shule ya sekondari ya wasichana Machame iliyopo mkoani Kilimanjaro na Swedi Shaury wa Makongo sekondari ya Dar es Salaam  ambao wamejishindia pesa taslimu shilingi laki moja na nusu 150,000 na vitabu vyenye thamani hiyo kila mmoja.

Katika mjadala wa jopo uliofanywa,  mwandishi  mkongwe Richard Mabala amesema  matumizi ya mitandao ya kijamii hususani facebook na whatsapp imekuwa kikwazo kikubwa kwa vijana katika kukuza uwezo wao wa kubuni na kuandika kwani wanatumia muda mwingi huko. Naye mkurugenzi wa Soma Bi Demere Kitunga amesema ni muhimu kuwa na fasihi yetu wenyewe ili kukuza utamaduni wetu, kwani kupitia fasihi tutaweza kurithisha utamaduni wetu kutoka kizazi kimoja hadi kingine na tusipofanya hivyo tutaishia kufuata utamaduni wa watu wengine. Akizungumzia shindano hili, Bi Demere amesema kwamba, shindano hili linalenga kuwafungua vijana na kuwajengea uwezo wa kuwa waandishi wazuri siku za usoni.

Matumizi ya mitandao ya kijamii hususani facebook na whatsapp yamekuwa kikwazo kikubwa kwa vijana katika kukuza uwezo wao wa kubuni na kuandika– Richard Mabala

 

Sherehe hizi ziliburudishwa na mwanamuziki Vitali Maembe na Lakini Chanzi. pia kulikuwa na ushairi kutoka kwa mwanafunzi Zawadi Suleiman kutoka shule ya sekondari Tambaza.

Hata hivyo sherehe hizi zilihitimishwa kwa mkurugenzi mtendaji – Soma kuzindua mzunguko wa nne wa Shindano hili (2016/2017) wenye dhima ya ‘Utandandawazi’ na kuomba wanafunzi wa sekondari kushiriki kwa kuandika hadithi zao na kuzituma kabla ya mwezi Februari kwisha.Ikumbukwe kwamba, halfa hii ilitanguliwa na warsha ya siku tano kwa wanafunzi waliofanikiwa kuingia 20 bora kwa ajili ya kuwafundisha mbinu za uandishi na kuwajengea uwezo wa kuboresha kazi zao ziweze kukubalika katika soko la fasihi. warsha hiyo iliendeshwa na walimu Elizabeth Mahenge kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam, Joram Nkya kutoka chuo kikuu cha kumbukumbu ya mwalimu nyerere na Mwandishi Elias Mutani.  Wanafunzi waliohudhuria warsha hiyo ni Buliba Magambo kutoka Benjamin W. Mkapa sekondari, Kulwa Abdallah – Makongo, Zawadi Suleiman – Tambaza, Swedi Shaury – Makongo, Aneth Mirambo – Ruvu, Maria Makasi – Jangwani, Jackline Kisanga – Machame girls, na Asha Malolo – Zanaki.