ua n (nyua), U-N-, mzizi maua
Nyuma ya Nyumba, Uzio
Muktadha: Inahusu nyumbani Uswahilini. Kimila, uani kawaida kuna uzio, na pametengwa kama sehemu maalum ya wanawake (ya ‘faragha’ na ‘salama’ mbali na ‘macho (ku mchuzi)’ ya wanaume ambao wao hukaa barazani na maeneo ya wazi mitaani.
Maelezo kuhusu mapendekezo:
- Ili kuunda dhana kuhusu maonyesho haya, ninaanza maelezo haya na mapishi ya keki maarufu ya Bibi yangu Mkunde:
Changanya kikombe 1 cha sukari na kikombe 1 cha siagi, koroga hadi sukari iwe nyepesi na laini. Mchakato huu unahitaji mkono wenye nguvu. Unawakilisha ukuaji/kukua na, kwetu sisi watoto, wengi wetu daima tulitamani kukua na kuwa na nguvu za kutosha ili siku moja tuweze kuchanganya sukari na siagi vizuri kama alivyoweza kufanya Bibi Mkunde kwa kutumia uma au kijiko cha kuchonga. Kisha, vunja na kuchanganya taratibu mayai matatu, moja baada ya jingine. Kabla ya kuweka yai la kwanza, inabidi uamue utazungusha mkono wako kuelekea upande gani unapokoroga – yaani kushoto au kulia. Bibi siku zote alisisitiza kuwa siri ya keki nzuri ni kutobadilisha mwelekeo wa mkono wako wakati wa kuchanganya mayai. Ni dhahiri kuwa mchakato huu ulichosha sana mkono yetu midogo.
Ukishachanganya mayai yote 3 unaweka vikombe 2 vya unga wa ngano, nao pia kikombe kimoja baada ya kingine. Kwa kila kikombe, kijiko kimoja cha baking powder huchanganywa kwanza na unga wa ngano kabla ya kuwekwa taratibu kwenye bakuli la kukorogea kwa kuchekecha. Katika hatua hii, tunaacha kutumia uma na mwiko. Badala yake tunatumia kisu kuchanganya unga taratibu hadi uwe mchanganyiko mzito usio na madonge. Baada ya hapo, unaongeza kikombe kimoja cha maziwa au maji ili kuulainisha mchanyato huo. Na mwishoni kabisa, kukoleza ladha, tunaweka kiasi kidogo cha sehemu ya nje ya maganda ya malimao yaliyosagwa (au vanilla kama unaweza kuipata). Hata hivyo, vanilla ni kiungo adimu ambacho Bibi Mkunde asingeweza kukipata kirahisi, hivyo siku zote ladha ya maganda ya malimao ndiyo ladha maarufu katika upishi wa keki wa Bibi.
Hii ni keki ya kawaida, yaani isiyo na vikorombwezo vingi. Lakini kwa wengi wetu katika familia yetu, keki hii ni zaidi ya kitu tunachokula na kusahau. Kila unapong’ata kipande cha keki hii unapata…
Hisia na kumbukumbu ya mambo ya kale inayonirudisha moja kwa moja jikoni kwa Bibi; ambapo tunapachukulia kama sehemu ya kuwa karibu na kujenga mahusiano (kati ya wanafamilia) na kusimuliana hadithi, historia, kufundishana mapishi, pamoja na roho ya ukarimu.
Kumbukumbu ya makuzi yangu mwaka hadi mwaka – tangu nikiwa msichana mdogo asiye na nguvu za kutosha kuchanganya sukari na siagi vizuri – jambo ambalo kwa kiasi kikubwa lilisababishwa na watu walionizinguka wakati wakati huo, na hata jumuiya pana (ya wanawake zaidi) inayoyazinga maisha yangu hivi sasa.
Pia huibua moyo wa kushikamana – wa kushikana mkono mmoja anapotetereka au kukwama. Ninapotetereka na kupata changamoto katika hatua mbalimbali za kuandaa keki, siku zote ni dada yangu na Mama Mdogo ambao walininusuru; kama ilivyo leo hii ambapo nina dada na mama wengi ambao wanaendelea kunilinda nisikwame. - Kutoka Uani/From the Backyard ni maonesho lakini pia ni pendekezo (la pamoja) linaloakisi maisha ya ujima na kutegemeana, thamani ya kushirikiana na kupokezana vijiti kutoka kizazi hadi kizazi, na utamaduni wa kurithishana (hadithi, historia, majina, zawada, ujuzi, upishi, mavazi na kadhalika); pia hutokana na urithi wa aina mbali mbali kutoka jikoni/mekoni, nyua, na sehemu zingine zinazojulikana kama ‘maeneo ya wanawake’ – kama vile jikoni kwa Bibi Mkunde – na desturi ya kuwa pamoja inayodhihirishwa na ‘matoleo’ yanayotoka kwenye maeneo hayo (kama kutafuna kipande cha keki maarufu ya Bibi Mkunde).
- Maonesho haya ni ya wasanii wanne ambao wametumia Sanaa za maonyesho na za maneno kuunda mchanyato wa hadithi, historia, sauti zilizokusanya kutoka kwenye michakato mbalimbali ya kusikiliza, kunusa, kuelewa na kuhusiana na, pamoja na kujiwekea nafasi stahiki nyakati zote.
- Sisi (wasanii na waandaaji wa maonesho) kwa pamoja tunawasilisha Kutoka Uani/From the Backyard kama pendekezo letu lenye maana pacha. Kwa upande mmoja, tunauibua na kuutambua ua (na ‘sehemu nyingine zinazotawaliwa na wanawake’) kama makavazi hai yaliyosheheni historia na maarifa ambayo aghalabu hutwezwa, hukandamizwa, na/au kunyamazishwa na kufifia; nusura yapotee kabisa kutokana na dhana kwamba ni ya kawaida. Kwa upande mwingine, ‘tunakemea’ uhafidhina unaotawala misingi ya sehemu hizo na kuhoji mazingatio ya mfumodume yanayoamua sehemu au mahali pa/alipotengewa mwanamke katika mfumo wa kudhibiti maarifa, utendaji na nafasi. Kwa hiyo, ni pendekezo linalowakilisha ‘kutwaa’ na ‘kusafisha’ mgando wa itikadi zilizokita mizizi katika nafasi (sehemu/maeneo) hizo—Kutoka Uani inaweza pia kueleweka kwa maana ya kutoka/kuachana na (au kupaweka huru) Uani/sehemu za wanawawake ‘tulizozizoea’ kama ‘sehemu za kujitenga na kuwekwa ndani’.
- Kutoka Uani/From the Backyard kama pendekezo pia linawasilisha mwanzo na mwisho.
Kama matokeo ya mwisho wa mradi wa Uliza Wahenga Dada! uliobuniwa kwa pamoja baina yangu na taasisi za Soma na Bookstop Sanaa (BSS); maonyesho haya yanahitimisha safari tuliyoianza na wasanii sita (waliochaguliwa kutoka kwenye orodha ya wateule 10). Pamoja nao na waratibu wa mradi, tulidhamiria kutafuta, na kuibua ushahidi wa michango anuwai ya wanawake isiyoonekana wala kutambulika katika kumbukumbu za kiutamaduni na kisisasa jijini Dar es Salaam na maeneo jirani ya mwambao. Bahari ya Hindi ilikuwa kitovu kikuu cha mradi, kama kavazi na pia kama eneo la marejeo. Kwa mwaka mmoja na nusu, wasanii hao walifundishwa na kuongozwa katika kujifunza mbinu/methodolojia mbalimbali za kitafiti pamoja na itikeli/maadili ya kufanya tafiti za kihistoria na kuzitafsiri kwenye kazi zao za sanaa. Katika kipindi hiki killa mmoja wao alijifunza kutoka kwa mwenzake walipokula pamoja, kutembea pamoja, kuruhusu hofu, mashaka na udhaifu wao uonekane (‘kufunguka’, kucheka, na kulia) kwa wengine. Waligundua pamoja (kwa njia ya ufukunyuzi) na kushirikiana ili hatimaye waibuke na hadithi ‘moja’, inayosimuliwa kwa mitazamo tofauti.
Kwa kuwa mawazo na miradi iliyotangulia ina tabia ya kuibuka tena na kujipenyeza kama maulizo katika michakato inayofuata, thana ya ua iliyorudiarudia rudia katika mazungumzo, tafiti, na michakato mbalimbali ya utekelezaji wa mradi wa Uliza Wahenga Dada! imeendelea kusumbua fikra zetu na kugusa nafasi zetu hadi imetufanya tubuni mradi mwingine ambao tumeuita Uani. Hivyo, maonesho haya yaufungua mwaka huu kama ua wa kwanza wa halaiki, ukiwa kifungua pazia cha mradi mpya wa Soma unaolenga kutengeneza nafasi za kubuni, kusanifu na kuratibu maonesho yenye kuibua kisanii na kuijenga upya nguvu ya kavazi la maarifa ya asili endelevu ambayo ndiyo Uani. - Ili kukomelea maonesho haya kifikra, namalizia maelezo haya na ‘matoleo’ mengine, safari hii kutoka kwa Mama, Demere:
Kama wafungwa wanavyotumia fundo za vidole vyao kula njama za kutoroka, hali kadhalika wanawake. Kwa uchungu. Kizazi hadi kizazi. Husuka ngano ya utoro. Chana kwa chana.
Uani wanapoalikwa
Kama ilivyo ada
Wapo wanaopata umahiri wa kujipendekeza
Na wa kurudishana nyuma
Wengine huchora njia ya kutorokea
Alama kwa alama
Kazi haziishi kuwazonga
Fundo za vidole zavuja damu
Ndimi zapinda
Njia za kutorokea zinafunguka
Ndani ya chana za mikeka na kawa
Njama zapangwa na kutamkwa
Toka kizazi hadi kizazi
Maelezo ya maonesho yameandaliwa na Rehema Chachage.
Wasanifu wa maonyesho: Demere Kitunga, Rehema Chachage, and Sarita Mamseri
Wasanii: Abigail Kiwelu, Asteria Malinzi, Liberatha Alibalio, and Ngollo Mlengeya
Tunawatambua: Hawa Ally, and Priscilla Mlay wasanii wetu wawili (wanaokamilisha timu yetu ya wasanii 6) wa Uliza Wahenga Dada! ila kwa bahati mbaya hawakuweza kushiriki maonyesho haya.
Shukurani nyingi ziwaendee Valeri Asiimwe Amani (Mratibu wa Mradi/ msanifu msaidizi wa maonesho na mwezeshaji wa mawasiliano na wasanii, Rahma Maabad (aliyekuwa mratibu wa mradi kwa muda mfupi), and Jesse Gerald msanifu wa hafla na ratiba ya ufunguzi.
Soma zaidi Kuhusu Maonesho haya:
Kutoka Uani/ From the Backyard Matamko ya Wasanii