Klabu ya Usomaji, inayotambulika kama Taswira “Book Club”, yenye maskani yake katika Mkahawa wa Vitabu, Soma, inaendelea kufanya vyema katika shughuli zake za kuhamasisha usomaji miongoni mwa WaTanzania. Soma, taasisi inayohamasisha usomaji nchini Tanzania, katika azma yake ya kuchagiza wanajamii kujijengea utamaduni wa kupenda kusoma na kuyasaka maarifa pamoja na Klabu ya Taswira zinaonekana kufanikiwa kwa kiwango kikubwa katika duru yake ya kujenga jamii yenye watu wenye ujuzi wa mambo na wenye kuhusudu maarifa.
Klabu ya Usomaji ya Taswira ilianza harakati zake za kujenga na kupeana hamasa ya kusoma vitabu miongoni mwa wanajamii mnamo mwishoni mwa Januari, 2016. Wadada watatu (Joan Kimerei, Asha Abdallah na Sauda Simba), wenye mapenzi ya dhati ya kujisomea, baada ya mazungumzo baina yao, waliamua kuanzisha kikundi cha watu wanaopenda kusoma baina yao ilimradi kuweza kupeana chachu ya kusoma na kisha kukutana kujadiliana juu ya vitabu husika. Kutokana na kuwiana kiazma na Soma, ndipo Klabu hiyo ikaingia katika ushiriki na Soma katika kueneza utamaduni wa kujisomea kwa kuwakutanisha wasomaji wa vitabu kutoka sehemu mbalimbali katika jiji la Dar es salaam; lengo ikiwa ni kusoma na kujadili kazi (fasihi) mbalimbali.
Klabu ya Taswira imeazimia kujikita zaidi (au tuu) katika kazi za fasihi za Afrika, yani zilivyochapishwa barani au kuandikwa na mwandishi wa barani. Kutokana na maazimiyo hayo, Klabu ya Taswira ikaanza utekelezaji wa shughuli zake katika mwezi wa pili, Februari, ambapo klabu hii hukutana katika viunga vya Soma katika kila Jumatano ya mwisho wa mwezi kujadiliana juu ya mada anuwai zilizojitokeza katika kitabu cha mwezi husika.
Mchakato wa mazungumzo na majadiliano ya vitabu ya Klabu ya Taswira yalianza mwishoni mwa mwezi Februari, Jumatano (24/02/2016). Kitabu kilichojadiliwa mwezi huo ni Stains in my Khanga kilichoandikwa na Sandra Mushi.
Safari ya usomaji kupitia Taswira imezidi kupamba moto kwa miezi sita sasa na hatimae kuweza kuvutia hisia za wengi juu ya majadiliano ya vitabu husika. Mpaka sasa washiriki wa klabu hiyo wameweza kusoma na kujadiliana vitabu vitano. Vitabu hivyo navyo ni Stains in my Khanga – Sandra Mushi; In the Belly of Dar es Salaam – Elieshi Lema; The Thing Around Your Neck – Chimamanda Ngozi Adichie; Parched Earth – Elieshi Lema na Broken Reed – Sophia Mustafa, katika mtiririko wa mwezi (kuanzia Februari mpaka Juni).
Kwa mwezi wa Julai, kikundi cha Taswira kitatimiza miezi sita kwa kusoma kitabu cha LONDON CAPE TOWN JO’BURG kilichoandikwa na muandishi kutoka Afrika Kusini – Zukiswa Wanner. Kitabu hiki kinapatikana Soma kwa Tshs. 30,000/=. Washiriki wa kikundi hiki watakutana siku ya Jumatano ya 27/07/2016 panapo Mkahawa wa Vitabu – Soma. Muda wa kukutana ni saa moja usiku na mazungumzo hufanyika kwa takribani masaa mawili na nusu hadi matatu (1900hrs – 2130hrs).
Klabu ya Taswira licha ya kujiwekea lengo la kuwa na idadi mahususi kwa ajili ya washiriki (baadae), bado iko huru kwa mtu yeyote kujiunga na kushiriki katika shughuli zake; ambapo kujiunga kwake ni bure, ila tuu usome kitabu husika cha mwezi (kwa kukinunulia Soma) na kisha ushiriki kweny mazungumzo juu ya kitabu hicho. Karibu ndugu. Mkaribishe na mwenzako.
Karibu tusome. Karibu tujadili. Karibu tushirikishane maarifa.
#Soma #Utamaduni #Burudani #Maarifa #TaswiraBookClub