Nani kuibuka kinara wa shindano la hadithi fupi kwa wanafunzi wa shule za sekondari – Andika na Soma?
Oktoba 10, 2015, shindano la hadithi fupi – Andika na Soma – lilifikia kikomo kwa kuwatunuku vinara wa shindano hilo katika hafla iliyofanyika katika viwanja vya Mkahawa wa Vitabu – Soma. Mwanafunzi Zahara Tunda, aliehitimu masomo yake katika shule ya sekondari ya wasichana Ruvu aliibuka kidedea baada ya kuwabwaga wanafunzi wenzake 307 walioshiriki shindano hilo, katika mzunguko wa pili wa shindano. Hadithi yake aliyoiita Uyoga ilichaguliwa kuwa hadithi bora miongoni mwa majaji watatu.
Kama inavyofahamika, safari moja huanzisha nyengine na mwisho wa safari moja ni mwanzo wa safari mpya. Kilele cha mzunguko wa pili kilichochea na kuanzisha mchakato wa mzunguko wa tatu ambao ulifunguliwa baada tuu ya kufungwa kwa mzunguko wa pili kwa kumpata mshindi. Hii ikafungulia njia kwa mwanafunzi mwengine kuvipokea viatu vya Zahara, mshindi wa mzunguko wa pili; na kuibua swali, Ni nani ataibuka kinara katika shindano hili?
Swali hili la msingi limeendelea kuziangaisha fikra zetu mpaka sasa. Wanafunzi walioshiriki wamekuwa na shauku ya kutaka kujua iwapo ni wao walioibuka vinara. Hadithi yangu imekuwa ya ngapi? Je nimeshinda? Maswali lukuki wamekuwa wakijiuliza na wengine hata wakituuliza. Hata hivyo hatimae jibu la swali hilo linakaribia kupatikana hivi karibuni.
Kati ya wanafunzi 107 walioshiriki katika mzunguko wa tatu, wanafunzi 20 wamechaguliwa kuingia 20 bora. Taarifa na mawasiliano ya wanafunzi hawa (20) zitawasilishwa shuleni kwao; na wanafunzi kumi (10) kati ya ishirini (20) watakaribishwa – kupitia shule zao – kushiriki kwenye warsha ya siku tano (5) inayolenga kuimarisha stadi zao za uandishi wa kubuni na kuboresha hadithi zao zifikie viwango vya kuweza kuchapishwa.
Kwa pamoja washiriki (wote) wa shindano hili wanakaribishwa kushiriki kwenye hafla ya kilele cha mzunguko wa tatu wa shindano la Andika na Soma – 14/10/2016. Hafla ya kilele itawawashirikisha pia viongozi na wadau mbalimbali wa elimu, na tasnia ya Kiswahili, fasihi na utamaduni; ambapo ratiba ya hafla itajumuisha kusomwa kwa kazi zilizoboreshwa pamoja na ugawaji tuzo kwa washindi. Tuzo zitagawawia katika nafasi tatu. Mshindi wa kwanza, wa jumla, na nafasi za mshindi wa pili na wa tatu zitagawiwa kwa jinsia zote mbili (ke na me). Hivyo kwa ujumla kutakuwa na washindi watano. Shule itakayotoa mshindi wa kwanza nayo itatunukiwa zawadi.
Licha ya kutanguliza shukurani kwa ushiriki wako na kutoa pongezi kwa ushiriki na ushindani mzuri, bado swali letu la msingi linabaki pale pale… Kati ya wanafunzi hawa ishirini (20) ni nani amefanikiwa kuibuka mshindi?
ORODHA YA WANAFUNZI WALIOFANIKIWA KUINGIA 20 BORA:
Makongo Secondary – Dar es Salaam
- Swedi Shaury
- Kulwa Abdallah
Ndanda Boys Secondary – Mtwara
- Said K. Said
Jangwani Secondary – Dar es Salaam
- Maria Makasi
- Irene Exavery Kivalu
Benjamin Secondary
- Buliba Magambo
Machame Girls Secondary
- Jackline Kisanga
- Upendo Mseli & Mariam T. Mwenesi (wameandika hadithi moja)
Masama Girls Secondary
- Diana Ewaldy
Tambaza Secondary
- Zawadi Suleiman
- Seif Ibrahim Chekanae
Loyola Secondary
- Ashiraph R. Mlaga
Kifungilo Secondary
- Julieth Samson Marwa
- Eliana Ludovick Swai
- Irene Ambrose Gindo
Ruvu Secondary
- Zela Kilawa
- Bethlove Steven
- Aneth Mirambo
- Hellen Natasha Kyatwa
Zanaki Secondary
- Asha Hassan Malolo