Katika azma ya kujenga jamii imara hatuna budi kushiriki na kushirikiana na watoto wetu katika shughuli zinazochangia maendeleo yao na ya jamii kwa ujumla.
Soma katika uratibu wa shughuli za watoto iliandaa michezo mbali mbali iliyowaburudisha watoto. Michezo hiyo pia iliwashirikisha wazazi wao. Kwa ujumla michezo na shughuli nzima ililenga kujenga ushiriki na mahusiano maridhawa baina ya wazazi na watoto.
Wikiendi na Watoto ilifana haswa kutokana shughuli mbalimbali zilizochagiza fikra za washiriki na kuwaburudisha. Shughuli hizo zilikuwa kivutio kikuu cha siku hiyo. Miongoni mwa shughuli hizo kulikuwamo na Masimulizi ya hadithi, mchezo wa kupuliza unga (kusaka kitu kilichomo ndani ya unga) na mchezo wa kutambua na kukumbuka vitu. Pamoja na michezo hiyo watoto walipata fursa ya kuimba na kucheza mziki, kucheza mpira na kupakwa rangi kwenye nyuso zao “face-painting”.
Siku hiyo iligubikwa na nyuso zenye furaha miongoni mwa watoto na wakubwa; huku ikiacha gumzo kubwa miongoni mwa wahudhuriaji. Pamoja na shughuli za burudani, kulikuwamo pia na maonyesho ya vitabu na vifaa vya watoto.